Na Peter Mwenda
MPANGO wa Taifa wa Damu Salama umekusanya chupa 8,480 za damu kati ya mahitaji ya mwezi Februari ya chupa 12,000 nchini.
Ofisa Uhusiano wa Mpango wa Damu Salama Tanzania, Bw. Rajabu Mwenda katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana alisema kuwa Kanda ya Mashariki yenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani,Dodoma na Morogoro iliongoza kwa kukusanya chupa 2,420.
Bw. Mwenda alisema Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mtwara na Lindi imeshika nafasi ya pili baada ya kupata asilimia 96 kwa kukusanya chupa 951 kati ya chupa 992 ambazo ilikuwa ikusanye na Kanda ya Nyanda za juu Kusini ilipata asilimia 77 baada ya kukusanya chupa 1,664 kati ya lengo la chupa 2,742.
Alisema Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Tabora, Kigoma na Singida imekusanya chupa 951 kati ya 1,962 na Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Tanga, Kilimanjaro,Manyara na Arusha imechangia chupa 997 katika ya chupa 1,808.
Ofisa Uhusiano huyo alisema Kanda ya mwisho ni Kanda ya Ziwa iliyochangia chupa 1,472 kati ya chupa 2,742 ambayo ni asilimia 54.
Alisema matumizi ya damu hiyo hutolewa bure katika hospitali mbalimbali nchini na kuongeza kuwa kati ya damu iliyokusanywa imekutwa na homa ya ini, virusi vya ukimwi na Kaswende.
Alisema kundi la wanaohitaji damu katika jamii ni watoto wadogo chini ya miaka mitano,mama wajawazito na wale wanaojifungua,wagonjwa wanaofanyiwa tiba ya upasuaji, majeruhi wa ajali mbalimbali na wagonjwa wenye upungufu wa damu kwa sababu mbalimbali kama vile kansa,Kifua Kikuu na Ukimwi.
Bw. Mwenda alisema bado kuna pengo kati ya damu inayokusanywa na mahitaji kwani hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pekee inahitaji wastani wa chupa 50 kwa siku.
Alisema mpango huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali za matumizi mabaya ya damu kidogo inayopatikana katika hospitali na miundo mbinu hafifu hususan barabara mbovu wakati wa ukusanyaji na usambazaji wa damu na
uuzwaji wa chupa za damu kunakofanywa na baadhi ya watumishi wa hospitali ambao si waaminifu hivyo kukatisha tamaa wachangia damu kwa hiari.
mwisho
No comments:
Post a Comment