Na Peter Mwenda
CHAMA Kipya cha Alliance For Democratic Change (ADC) kimewasilisha fomu za usajili wa muda katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania.
Mwenyekiti wa ADC, Bw. Said Miraji Abdallah na Katibu Mkuu wake Bw. Kadawi Lucas Limbu wakiwa na baadhi ya wafuasi wao waliwasilisha fomu hizo jana.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Msajili wa Vyama, Mwenyekiti wa ADC Bw. Said Miraji Abdallah alisema wameamua kuanzisha chama kipya kwa sababu vingine vyote havina mwelekeo wa kutatua kero za watanzania.
Alisema ADC ni chama ambacho kiko wazi na kukaribisha wengine wanaotaka kuleta mabadiliko ya watanzania wajiunge na chama hicho.
Wakiwa na mafuasi wao walikabidhi rasimu ya katiba ya ADC kwa mwangalizi wa wa Ofisi ya Msajili wa vyama pamoja na rasimu ya katiba yao ambazo zitakabidhiwa Mwanasheria ambaye atazipitia na kama zinahitaji marekebisho yafanyike.
"Kawaida sisi (mwangalizi wa ofisi ndiyo tunapokea fomu za kuomba usajili na kuziwasilisha kwa Mwanasheria ambaye atazipitia kama zinakasoro zifanywe" alisema Bi. Simbachawene.
Awali Bw. Said alisema amewahi kuwa kiongozi wa ngazi za juu wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa miaka mingi lakini ilipofika mwaka 2008 alijivua madaraka aliyokuwa nayo na kubaki mwanachama wa kawaida kabla ya kuungana na wenzake kuanzisha chama hicho.
Alisema chama hicho kinakaribisha wabunge wote waliofukuzwa katika vyama vyao akiwemo Mbunge wa wawi Bw. Hamad Rashid Mohamed na Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila kutetea haki za wananchi.
Bw. Said alisema ADC sera zake ziko wazi ambako hata Rais Jakaya Kikwete anakaribishwa kujiunga kwa sababu mwelekeo wake uko katika kubadilisha maisha ya wanyonge.
Naye Katibu Mkuu wa muda Bw. Limbu aliyewahi kugombea Ubunge Jimbo la Temeke kupitia CUF alisema wameamua kuanzisha chama kwa sababu wamechoshwa kuona hakuna sera zinazotekelezwa na vyama vingine.
Mmoja wa wanachama wa chama hicho, Bi.Leila Hussein ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF wilaya ya Kinondoni alisema wafuasi wa ADC ni wale waliokuwa CUFa ambao wamejing;atua baada ya kuona hakuna dhamira ya kweli ya kuwakomboa watanzania.
Alisema ADC ni chama kitakachiungwa mkono na watanzania wengi wakiwemo watu wazito serekalini ambao wamechoshwa na mwenendo mbovu wa vyama vingine.
mwisho
No comments:
Post a Comment