Na Peter Mwenda
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeishauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuanzisha mfuko maalum utakaotumika kwa ajili ya uchaguzi badala ya kutegemea wafadhili.
Mwenyekiti wa PAC, Bw. John Cheyo akizungumza katika kikao cha kamati ya bunge kupitia hesabu za Tume ya taifa ya Uchaguzi jana Dar es Salaam alisema mfuko huo ukianzishwa utaondoa omba omba inayofanywa kila inapofika kipindi cha uchaguzi na wakati mwingine wafadhili hao kuingia mitini kinapokaribia kipindi hicho.
"Uchaguzi Mkuu unafanyika kila baada ya miaka mitano,badala ya kutegemea wafadhili kwa nini tusidundulize fedha kidogo kidogo ili kujitegemea wenyewe badala ya kusubiri wafadhili ambao wanaweza kuingia mitini dakika za mwisho" alisema Bw. Cheyo.
Katika kikao hicho Makamu Mwenyekiti wa PAC, Bi. Zainab Vullu alihoji sababu za vituo kuwekwa mbali na wananchi na wengine kutaka kujua sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi katika baadhi ya vituo kwa kukosa vifaa vya kupigia kura, wananchi wengi kujiandikisha kupiga kura lakini wanaojitokeza wachache na kutongezwa kwa wapiga kura katika daftari katika chaguzi ndogo.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, Bw. Julius Mallaba alisema NEC imepanga kurekebisha kasoro hizo lakini inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na fedha za kutosha kushughulikia mambo ambayo yanatakiwa kurekebishwa katika tume ikiwemo watumishi wachache.
Alisema NEC haiwezi kugawa majimbo ya uchaguzi kwa sababu idadi ya wabunge katika majimbo yaliyopo wamefika kikomo hivyo ili kuwafikia wananchi wengi tume hiyo inatarajia kuongeza vituo vya kupigia kura kutoka 24,919 mpaka 60,000.
Alisema katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru daftari la wapiga kura litakalotumika ni lile lile lililotumika katika uchaguzi Mkuu wa 2010 na kuahidi kuwa uchaguzi ujao hakutakuwa na idadi kubwa ya wananchi kushindwa kupiga kura kutokana na kukosa majina yao kwa sababu utatumika mpango wa kujua kituo kutumia simu ya mkononi.
Kamati ya PAC ilidhinisha matumizi wa NEC na kuwataka wajipange kuhakikisha chaguzi zinazofuata hazina malalamiko ya matokeo wala kushindwa kupiga kura kwa sababu ya kukosa vifaa au kukosa majina yao kwenye orodha ya wapiga kura.
mwisho
No comments:
Post a Comment