Na Peter Mwenda
CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimelitaka Jeshi la Polisi Tanzania kuweka bayana amri iliyotoa ya kuzuia maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima kama inakihusu Chadema peke yake au pamoja na vyama vingine vya upinzani nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Bw. Julius Mtatiro akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alisema kauli ya Kamishna wa Operesheni Maalum na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Bw. Paul Kagonja kuzuia maandamano na mikutano nchini imesababisha usumbufu mkubwa kwa chama chake ambacho kimejipanga kufanya ziara nchini.
"Jeshi la polisi kama wanadhania kuna vyama vinafanya vurugu basi washughulike na vyama hivyo lakini si kutoa amri ya jumla wakati vyama vingine hajihusishi na vurugu" alisema Bw. Mtatiro.
Alisema CUF ambayo imepanga ziara ya mikutano katika mikoa ya Tabora, Tanga, Mwanza, Mtwara na Lindi, amri zinazotolewa zinasababishia usumbufu mkubwa na kupokea simu nyingi kutoka mikoani kuulizia kama wanahusika.
Bw. Mtatiro alisema jeshi la polisi limeshindwa kufafanua kuzuia maandamano yanamhusu nani na amri hiyo ilitolewa kwa maana gani katika nchi ya watanzania ambayo kuna vyama vingi vya siasa.
Bw. Mtatiro alisema serikali pia inaopaswa kutoa kauli kuhusu ujio wa mtoto wa Mfalme wa Uingereza, Prince Charles kuingia nchini wakati Waziri wake Mkuu, Bw. David Cameroon kuzitaka nchi za Jumuiya ya Madola kukubali ushoga ili zinufaike na misaada ya Uingereza.
"Mwalimu Nyerere ameondoka na kila kitu chake, kama angekuwa hai Prince Charles asingethubutu kuingia nchini kutokana na kejeli za kishoga zilizotolewa na Uingereza wakati Tanzania tunao uwezo wa kujitosheleza kwa uchumi" alisema Bw. Mtatiro.
Alisema Serikali ya Rais Kikwete inakwenda chini kwa maana kuwa uchumi umeshuka na hakuna fedha za kuendesha nchi kulipa mishahara, kulipa ruzuku na nyingine.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Bw. Shaweji Mketo alisema chama hicho hakijapata ruzuku ya mwezi Oktoba ambayo inatakiwa kulipwa na Serikali kila tarehe 25 ya mwezi lakini hadi jana walikuwa hawajapata.
"Hata CCM walinipigia simu kuniuliza kama sisi (CUF) tumepata ruzuku na mimi nikawambia hatujapata" alisema Bw. Mketo.
Kamishna wa Polisi Bw. Kagonja juzi akitoa taarifa ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya Chadema nchi nzima baada ya jeshi hilo kupata taarifa kuwa mikutano hiyo itaharisha amani.
mwisho
No comments:
Post a Comment