Na Peter Mwenda
MWENYEKITI wa NCCR Mageuzi, Bw. James Mbatia ameiomba Serikali itenge siku moja kila mwaka itakayotumika kwa ajili ya wananchi kujitokeza kuchangia damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya watoto na watanzania wanaohitaji huduma hiyo.
Akizungumza baada ya kutoa damu katika kituo kidogo cha kutolea damu cha Mnazi Mmoja jana, Bw. Mbatia ambaye amekuwa akitoa damu mara kwa mara alisema kundi linalohitaji damu kwa wingi ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.
Alisema watoto wanahitaji damu asilimia 50, asilimia 30 inahitajika kwa ajili ya wajawazito, asilimia 15 kwa ajili ya ajali na asilimia 5 kwa ajili ya wagonjwa wa saratani.
Alisema ili kufikia malengo ya kuchangia damu mikakati hiyo ifanywe kitaifa kama ilivyofanyika upimaji wa virusi vya Ukimwi iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambako wananchi walihamasika kupima virusi kwa hiari.
"Watanzania walihamasika baada ya kumuona kiongozi wao wa nchi akipima virusi vya Ukimwi hivyo ili kuchangia damu kunahitajika hamasa kama aliyowahi kuifanya Rais Kikwete" alisema Bw. Mbatia.
Alisema wizara ya afya na Ustawi wa jamii inayo jukumu kuifanya siku hiyo kuwa ya kuokoa maisha ya watanzania na utoaji huo unaweza kuanzia bungeni ambako kutachochea wananchi wengi kujitokeza kutoa damu.
Alisema damu aliyotoa jana ambayo ni uniti moja inaweza kuokoa maisha ya watoto watatu lakini bado mahitaji ya damu kitaifa ni makubwa kuliko makusanyo.
Alisema mahitaji ya damu nchini kwa mwaka mmoja kunahitajika uniti 400,000 lakini zinazopatikana ni uniti 20 ambazo hazitoshelezi mahitaji.
Bw. Mbatia alisema makundi ya watu mbalimbali kwenye jamii wanatakiwa kuhamasika kutoa damu kwa hiari ili kukidhi mahitaji ya siku Jiji la Dar es Salaam ni uniti 140 na Hospitali ya Mihimbili inahitaji uniti 50 kwa siku.
Ofisa Uhusiano wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Bw. Rajabu Mwenda alisema ukusanyaji wa damu katika kituo chga Mnazi Mmoja ni uniti 3-5 kwa siku hivyo kuwahamamisha wananchi wengine kujitokeza kutoa damu.
mwisho
No comments:
Post a Comment