Na Rachel Balama
MEYA wa Jiji la Dar es Salaama Dkt. Didas Masaburi, ameiagiza Bodi ya sasa ya Jengo la Machinga Complex kuwafukuza wafanyabiashara walipewa vizimba vilivyokuwa chini ya Bodi ya awali iliyokuwa inaongozwa na Mwenyekiti wake Mbunge wa Jimbo la Ilala, Bw. Mussa Azzan Zungu ambao hawafanyibiashara na kugawa visimba hivyo kwa wafanyabiashara ambao ni machinga au kutangaza tenda kwa wenye maduka makubwa.
Mbali na kutoa maagizo hayo Dkt. Masaburi pia aliitaka bodi hiyo kumpelekea orodha ya majina ya wafanyabiashara kwenye visimba vilivyo chini ya bodi pamoja na mikataba ili aweze kupitia upya na kuona kama kuna mchezo mchafu ulitumika kuivunjilia mbali.
Dkt. Masaburi alitoa maagizo hayo Dar es salaama jana wakati alipofanya ziara ya ghafla katika jengo hilo kutokana na malamamiko kwamba ugawaji wa vizimba vilivyo chini ya bodi umefanyika kinyume na taratibu na kwa upendeleo.
Alisema kuwa kutokana na ugawaji wa vizimba hivyo kuwa wa kimagumashi ndio maana asilimia kubwa ya vizimba havijawekwa biashara.
"Hapa inaonekana kuna mchezo mchafu kwani inawezekana kabisa hapa kuna watu wamepewa na hao hao wakapangisha kwa wengine au huenda vizimba hivi ni vya watu wakubwa," alisema Dkt. Masaburi.
Hata hivyo katika ziara hiyo Dkt. Masaburi alishindwa kupata ufafanuzi toka kwa Meneja wa jengo hilo. Bi. Tedy Kundy kama vizimba hivyo vya bodi vinalimikiwa na wafanyabiashara ambao wapo kwenye mikataba kutokana na utofauti uliojitokeza wa majina ya wafanyabiashara waliokuwepo kwenye vizimba majina yao kutokuwa kwenye orodha ya wafanyabiashara wahusika walioorodheshwa na bodi.
"Ninaiagiza bodi kufanya yafuatayo, kwanza kuwafukuza wale wote waliogaiwa vizimba na bodi iliyopita ambao hadi sasa hawafanyibiashara na pia niletewe orodha ya wafanyabiashara wote pamoja na mikataba yao ili kuangalia uhalali kwa kuwa kuna minongono kwamba vizimba vilivyogaiwa na bodi waligawana kindugu na mbaya zaidi wengine wamewapangisha watu wengine kitu ambacho si sahihi," alisema Dkt. Masaburi.
Alisema kuwa wengi wa watu waliopewa vibanda hivyo hawajulikani hata kwa majina pia hawajulikani wataanza lini kufanyabiashara na mbaya zaidi vizimba vichache ndivyo vinalipa ushuru na asilimia kubwa hawalipi kutokana na kutokuwa na biashara jambo ambalo linasababisha kukosekana kwa mapato.
Alisema kuwa jengo hilo limejengwa kwa mkopo wa fedha taslim sh. bilioni 34 na Shirika la Nyumba nchini(NSSF) na haijulikani fedha hizo zitalipwa lini kutokana na jengo hilo kutoingiza kwa kuwa wafanyabiashara wamefunga vizimba na makufuli pasipo kufanya biashara.
Pia Dkt. Masaburi, alitoa agizo kwa bodi hiyo mara ya kuwaondoa wafanyabiashara hao kutangaza tenda ili wafanyabiashara waweze kushindana kwa vigezo au kama kuna uwezekano vizimba vya ghorofa za juu kuwapangisha hata wafanyabiashara wakubwa ili kuleta tija kwenye jengo hilo ikiwa ni pamoja na hata kuweza kuweka lifti.
"Angalieni uwezekano wa ghorofa za juu kuwapangisha wafanyabiashara wenye maduka makubwa kama(Supar market) kwani nao wanaweza hata kuongeza ufanisi kwenye majengo kwa kuweka hata lifti,"alisema Dkt. Masaburi.
Hata hivyo Dkt. Masaburi alisema kuwa anachofahamu vizimba vilivyopo chini ya bodi ni vizimba 549 lakini alishangazwa na meneja wa jengo kumueleza kwamba bodi ilipewa vizimba 348 tu.
Pia aliitaka bodi kuangalia uwezekano wa kuondoa nyaya kwenye visimba hivyo kwa kuwa hazileti muonekano mzuri na mbaya zaidi si kila biashara ipachikwe kwenye nyaja.
Alisema kuwa hakuona sababu ya vizimba vyote vilivyopo kwenye jengo hilo kuwekwa nyaja ambazo zimegharibu zaidi ya sh. bilioni moja.
Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara mbalimbali walimlalamikia Meya huyo kwa kile walichodai kwamba wafanyabiashara hawataweza kufanyabiashara kwa kuwa asilimia kubwa ya vizimba vilivyopo chini ya bodi vimefungwa kufuli pasipo kuwekwa biashara huku wafanyabiashara wengine wakiangaika kwa kutokuwa na nafasi kwa ajili ya kufanyabiashara.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara Walemavu Mkoa wa Dar es salaam,Bw. Kidumke Mohamed, alimtaka Dkt. Masaburi kuangalia uwezekano wa kulivunja soko la Mchikichini ili wafanyabiashara hao kwenda kufanyabiashara kwenye jengo la machinga ambapo meya alimueleza kwamba soko la Ilala lipo chini ya Manispaa hivyo atakaa na uongozi huo ili kuangalia kama kunauwezekano wa kufanya hivyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment