Na Peter Mwenda
WAKATI pilikapilika za uchunguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Igunga lililoachwa wazi na Bw. Rostam Aziz baada ya kujiuzulu, Bi. Isabela Makeremo (33) amejitokeza kuwa mgombea pekee mwanamke kutangaza kuchukua fomu kupitia Chadema.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutoka Igunga, Bi. Isabela alisema ameamua kugombea ili kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo kutatua changamoto mbalimbali ambazo kwa sasa zimekomaa na kuota mizizi.
"Ninyi mashaidi kuwa jimbo la Igunga kwa kipindi kirefu sasa limekuwa likichorwa kama jimbo lililozaa watu wenye sifa na wasifu mbaya wa ubadhirifu wa mali za umma na kashfa za kifisadi alizokuwa nazo mbunge aliyejihuzulu"alisema Bi.Isabela.
Alisema anauchungu mkubwa na jimbo hilo kwa sababu ni mzaliwa na
na mkazi wa kata ya Ziba wilayani Igunga hivyo atajitahidi kukuza ustawi wa wananchi wa jimbo hilo katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii ili kurudisha hadhi na heshima mbele ya jamii ya watanzania.
Alisema atatumia uwezo na ushawishi katika kuunda na kuhamasisha vikundi mbalimbali vya kijamii hususani wanawake na vijana kushiriki katika ujenzi wa ukuaji wa uchumi kuhakikisha wanapata kipato kinachoendana sawa na kazi ama bidhaa wanazozalisha.
Bi. Isabela alisema anaamini kuwa kutumia falsafa ya tutashinda, yupo tayari kutumia muda na akili kushirikiana na wananchi katika shuguli za kila siku za kiuchumi na kuwajengea uwezo ili kuhakikisha maendeleo ya wananchi hao yanapatikana.
“Wilaya ya Igunga wananchi wake wamekata tamaa ya maisha kutokana na mrundikano wa shida, umasikini, hali ngumu ya maisha, unyanyaswaji wa wafanyabiashara wakubwa dhidi ya wananchi masikini,utozwaji wa kodi na michango mbalimbali ya manyanyaso na katika jamii"alisema Bi. Isabela.
Alisema wakulima na wafanyabiashara hawana uhakika wa soko la bidhaa zao, panahitajika mtu wa kuchukua hatua madhubuti haraka iwezekanavyo, na ndio maana ameamua kujitoa kwa ajili ya kuwasimamia na kuwatetea wananchi wa Igunga.
Mgombea huyo alisema kutokana na elimu aliyonayo ya shahada ya kwanza sayansi ya kilimo ya Chuo Kikuu cha kilimo SUA, ni mwanasiasa na mwanachama wa CHADEMA kwa takribani miaka 5 sasa na mwanaharakati wa maendeleo katika sekta ya kilimo na wajasiriamali yaani wafanya biashara wa dogo na wa kati.
Alisema ameamua kuomba ridhaa ya chama chake cha Chadema ili awakilishe katika uchaguzi huo na awawakilishe wananchi wa wilaya ya Igunga katika bungeni.
Alisema kuzingatia ukweli kuwa ni mmoja wa wana Igunga ambao wana mapenzi thabiti na wilaya hiyo chama chake kitampitisha kuwa mgombea wa ubunge atakayetumia ushawishi wa muda mrefu katika kuwezesha chama kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment