TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Sunday, 21 August 2011

Mtoto wa miaka minne ateketeza nyumba yao kwa moto

Na Peter Mwenda

FAMILIA sita zenye watu 21 hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba walimokuwa wakiishi eneo la Kitunda kwa Nyangasa kuteketea kwa moto baada ya mtoto Albert Nicolaus (4) kuchoma godoro.

Watu walioshudia tukio hilo walisema moto huo ulisambaa kwenye nyumba hiyo kwa kasi mbali ya jitihada za majirani kuokoa mali zilizokuwepo kushindikana, mali za vyumba vya nje ndivyo vilivyosalimika.

Mama wa mtoto Albert, Bi. Neema Nicolaus ambaye hakuwepo nyumbani wakati wa tukio  hilo alisema alipata taarifa kutoka kwa Housigeli wake, Bi. Jasmin Nurdin (18) kuwa mwanaye amechoma nyumba na kuteketea.

Alisema katika nyumba yake hiyo vitu vyake vyote na mpangaji wake mmoja vimeteketea kabisa zikiwemo fedha taslimu sh. mil. 1. 7 ambazo alikuwa akanunue bidhaa kwa ajili ya kuuza kwa jumla dukani kwake.

Bi. Neema ambaye ni mjane aliyefiwa na mumewe Nicolaus mwaka jana, alisema hajui aanzie wapi kwa sababu maisha yake yalitegemea wapangaji kulipa kodi na mradi wa duka ambao msingi wake umeteketea kwa moto.

Mjumbe wa shina Bw.Omari Banza alisema mtoto huyo hilo ni tukio lake la pili baada ya lile la kwanza siku nne zilizopita alichoma moto chandarua lakini kabla ya kusambaa sehemu nyingine majirani waliuzima.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mzinga, Bi. Flora Lemu alisema walijitahidi kupiga simu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuomba msaada wa gari la kuzima moto lakini hawakupata msaada kwa wakati ambako baada ya saa moja na nusu kupita ndipo lilifika huku nyumba ikiwa imeteketea.

Diwani wa Kata ya Kitunda, Daniel Ryoba alisema mama huyo na wapangaji wake zaidi ya watu 21 wanahitajki kusaidiwa ili kurejea katika maisha yao ya awali.

Alisema wasamaria wenye nia ya kumsaidia mama huyo wanaweza kuwasiliana naye kupitia ofisi ya Manispaa ya Ilala. 

mwisho



No comments:

Post a Comment