Na Peter Mwenda
CHAMA tawala CCM kimekiri kuwa kuna baadhi ya watumishi wa umma ambao si waaminifu na kuvujisha siri za Serikali.
Akizungumza katika mahafali ya 23 ya Chuo cha Biashara na Uhazili cha Splendid, Dar es Salaam juzi Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Kilumbe Shaaban Ngienda alisema taaluma ya uhazili ina maadili yake ya kutunza siri za ofisi hivyo chama hicho hakina sababu ya kuendelea kuwakumbatia wafanyakazi waovu.
Alisema ni kweli risala ya wanachuo 98 waliohitimu katika chuo hicho na kuongeza kuwa wafanyakazi wa serikali wengi wanavujisha siri wataondolewa na kuwekwa wenye maadili ya taaluma zao.
Bw. Kilumbe alisema wapinzani wamekuwa wakitumia visingizio vya maandamano kupinga Serikali ya CCM lakini wajue kuwa hiyo si njia ya kutatua kero za wananchi hivyo wanatakiwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi badala ya kutafuta visingizio.
Alisema CCM imejipanga kuchukua Jimbo la Igunga na lazima italichukua kwa sababu wananchi wanakipenda chama hicho kwa sababu ndicho kinawakomboa katika matatizo mbalimbali ya elimu, uchumi na kuendelea kuwajengea amani.
Bw. Kilumbe aliahidi kuwatafutia ajira wahitimu hao katika ofisi za chama ngazi ya wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke na kutoa komputa mbili na mashine za kuchapa (Type Writer) mbili kwa ajili ya chuo hicho.
Awali Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Caasim Taalib alisema chuo hicho kinatoa nafasi kumi kwa vijana wa CCM kusoma bure kozi ya Uhazili katika chuo hicho na kati ya wahitimu hao 65 wamekubali kujiunga na CCM na kuacha vyama vyao vya Chadema na CUF.
mwisho.
No comments:
Post a Comment